Baada ya kushindwa muswada wa azimio kuhusu Syria mbele ya baraza la Usalama, Saudi Arabia inataka hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa ilishughulikie suala la hali namna ilivyo katika nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha CNN, viongozi wa Saudi Arabia wanapanga kuwasilisha muswada wa azimio mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa. Muswada huo unalaani vikali jinsi serikali ya Syria inavyovunja haki za binaadam. Jumatatu ijayo, mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Haki za binaadam ya Umoja wa Mataifa Bibi Navy Pillay anapanga kuzungumza mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali namna ilivyo nchini Syria. Kwa mujibu wa makundi ya upande wa upinzani mapigano yameripuka upya kati ya makundi ya wapinzani na yale ya wafuasi wa Rais Bashar al Assad hii leo ambapo watu wasiopungua 26 wameuwawa. Katika ngome ya wimbi la mageuzi watu 20 wanasemekana wameuliwa-wengine sita wameuliwa katika vitongoji vya mji mkuu Damascus. Mapigano yameripuka pia karibu na mji mkuu, kati ya vikosi vya serikali na wanajeshi walioasi.
Maandamano na mgomo jumla ulioitishwa na mashirika yanayopigania masilahi ya wafanyakazi, kulalamika dhidi ya hatua za kufunga mkaja, yamezifanya zipooze shughuli za maisha kwa siku ya pili nchini Ugiriki. Shughuli za usafiri wa mabasi, tramu na vivuko zimesita. Maandamano pia yanategemewa kufanyika hii leo. Machafuko yalizuka katika maandamano ya jana ambapo watu wanane walijeruhiwa. Kabla ya hapo baraza la mawaziri la Ugiriki liliidhinisha mpango wa kufunga mkaja uliofikiwa pamoja na wafadhili wa kimataifa na kwa namna hiyo kuinusuru Ugiriki isifilisike. Bunge linatazamiwa kukutana baadae kesho usiku kwa kikao muhimu kilicholenga kuidhinisha mpango huo wa hatua za kufunga mkaja.
Upande wa upinzani umeitisha mgomo na maandamano ya umma hii leo kuadhimisha mwaka mmoja tangu kiongozi aliyeitawala Misri kwa muda mrefu, Hosni Mubarak alipong'olewa madarakani. Kwa namna hiyo makundi zaidi ya 30 ya upande wa upinzani yanataka kulishinikiza baraza tawala la kijeshi liwakabidhi raia hatamu za uongozi. Mwito huo wa mgomo umekosolewa hata hivyo tangu na waumini wa Kiislam mpaka na viongozi wa dini ya Koptik. Chama cha Udugu wa Kiislam kilichojipatia ushindi mkubwa katika uchaguzi uliopita wa bunge kimesema hakitoshiriki katika maandamano yoyote ambayo yatafuja shughuli za kiuchumi za Misri.Baraza tawala la kijeshi limepinga kwa mara nyengine kukabidhi mapema hatamu za uongozi kwa raia. Wakati huo huo vikosi vya jeshi vimekuwa vikionekana katika kila pembe ya nchi hiyo. Vifaru na wanajeshi wanalinda taasisi na njia kuu pia.
Licha ya shinikizo linalozidi kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya,Rais Mahmoud Ahmedinedjad ametangaza hii leo mradi mpya wa kinuklea. "Mnamo siku zinazokuja, ulimwengu utashuhudia kuzinduliwa mtambo mwengine wa kinuklea nchini Iran", amesema Rais Ahmedinedjad alipokuwa anafunga mkutano wa hadhara mjini Teheran kusherehekea mapinduzi ya Kiislam ya mwaka 1979. Hakutoa maelezo zaidi. Marekani na Umoja wa Ulaya zinaiwekea Iran vikwazo ili kuilazimisha nchi hiyo iachane na mpango wake wa kinuklea. Iran inatuhumiwa kutengeneza silaha za kinuklea.
Waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Dirk Niebel amezungumzia uwezekano wa kusitishwa vikwazo dhidi ya Burma pamoja na kuwajibika kwa nguvu Ujerumani katika kuijenga upya nchi hiyo. Mwanasiasa huyo wa kutoka chama cha Kiliberali cha FDP ameliambia gazeti la "Leipziger Volkszeitung", masharti ya kuondolewa vikwazo vya kimataifa na hasa vikwazo vya Umoja wa Ulaya ni pamoja na kuitishwa uchaguzi huru na wa haki, suluhu ya kitaifa pamoja na makundi yote ya jamii za wachache na kuachiwa huru wafungwa wote wa kisiasa waliosalia. Waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Dirk Niebel ni waziri wa kwanza wa Ujerumani kuitembelea Burma tangu mwaka 1984. Anasema anataka kujionea maendeleo yaliyoweza kupatikana katika utaratibu wa kuleta demokrasia katika nchi hiyo inayoongozwa na wanajeshi. Waziri Niebel amepanga pia kukutana na kiongozi wa upande wa upinzani Bibi Aung San Suu Kyi. Ujerumani imesitisha ushirikiano wa maendeleo pamoja na Burma tangu wanajeshi walipotumia nguvu kutawanya maandamano ya wanafunzi mnamo mwaka 1988.
Sudan na Sudan Kusini zimeombwa ziregeze misimamo yao katika ugomvi kuhusu mafuta, siku moja baada ya pande hizi mbili kufikia makubaliano kuhusu mgogopro wao wa mpaka. "Tunaiomba Sudan Kusini ianze upya kuchimba mafuta na tunaziomba pande zote mbili zisitishe uamuzi wa upande mmoja" amesema hayo msimamizi wa mazungumzo hayo, Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya. Ametoa mwito wa kufikiwa maridhiano katika wakati ambapo mazungumzo yaliyoanza katika mji mkuu wa Ethiopia - Addis Abeba kati ya Sudan na Sudan Kusini, yanatarajiwa kuendelea hadi Jumatano. Mazungumzo hayo yanasimamiwa na Umoja wa Afrika. Ufanisi umepatikana jana usiku katika mazungumzo hayo pale Sudan na Sudan kusini zilipokubaliana kusitisha uchokozi katika eneo la mvutano la mpakani.
Baraza la mpito la taifa nchini Libya limeitolea mwito serikali ya Niger iwakabidhi Saad Gaddafi, mtoto wa kiume wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi na familia ya kiongozi huyo aliyeuliwa. Madai hayo yametolewa baada ya Saad Gaddafi kukiambia kituo cha televisheni cha Al Arabia anataka kurejea nchini kwa hoja kwamba asilimia 70 ya wananchi hawaridhiki na hali namna ilivyo hivi sasa.Niger imeukataa mwito huo. Hata hivyo imeomba radhi kwa viongozi wa Libya kutokana na Saad Gaddafi "kuyaendeya kinyume masharti ya ukimbizi." Niger imemkubalia Saad Gaddafi kinga ya ukimbizi" kwa sababu za kiutu."
Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.de.