| 09.05.2008 | 14:00 UTC
Mji wa Beirut wakosa watu wakati wafuasi wa Hezboullah wakithibiti sehemu ya magharibi ya mji huo.
Beirut.
Rais wa Syria Bashar al-Assad ameueleza mzozo wa kisiasa nchini Lebanon kuwa ni suala la ndani ya nchi hiyo ambalo linapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo.
Taarifa ya Assad , ambayo imeripotiwa na vyombo vya habari nchini humo, inakuja katika siku ya tatu ya mapigano baina ya upande wa upinzani unaongozwa na Hezboullah na wafuasi wa serikali.
Wanamgambo wa Hezboullah hivi sasa wanadhibiti eneo kubwa la magharibi ya Beirut, wakati uwanja wa ndege umefungwa pamoja na bandari kuu ya mji huo kutoweza kufanya kazi.
kituo cha televisheni kinachounga mkono serikali cha Future News pia kimeshindwa kutoa matangazo yake.
Wakati huo huo wizara ya mambo ya kigeni ya Italia imetangaza kuwa inajitayarisha kuwaondoa raia wake kutoka Lebanon. Ghasia hizo zimezuka baada ya serikali kutangaza kuwa mfumo wa mawasiliano wa kijeshi wa kundi la Hizboullah ni kinyume na sheria. Kiongozi wa Hezboullah Hassan Nasrallah amesema kuwa uamuzi huo wa serikali unamaanisha kutangaza vita.
Ujerumani imetoa wito leo wa kumalizwa mara moja kwa hali ya kukosekana kiongozi nchini Lebanon , na kusema kuwa hali hiyo inazidisha wasi wasi ambayo inaisukuma nchi hiyo katika ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema baada ya kuzungumza kwa simu na waziri mkuu wa Lebanon Fouad Siniora kuwa ana wasi wasi mkubwa kuhusiana na mapigano hayo kati ya Wasunni wanaounga mkono serikali inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi na wapiganaji wa Kishia.






