News | 09.05.2008 | 14:00 UTC
Utawala wa kijeshi wa Burma waendelea kukataa misaada ya nje.
Rangoon.
Licha ya mbinyo mkubwa wa kimataifa dhidi ya utawala wa kijeshi wa Burma kukubali misaada kutoka nje, utawala huo unaendelea kukataa misaada hiyo ya kiutu.
Msemaji wa mpango wa chakula wa umoja wa mataifa amethibitisha kuwa shirika hilo limesitisha safari zote za anga za kupeleka misaada nchini Burma wakati ikiendelea na majadiliano na utawala wa nchi hiyo kuweza kuruhusu misaada kuingia nchini humo.Kamishna wa misaada ya maendeleo wa umoja wa Ulaya Louis Michel amesema leo kuwa hatua hiyo ya Burma haikubaliki kabisa.
Katika taarifa leo Ijumaa wizara ya mambo ya kigeni ya Burma imesema kuwa haiko katika nafasi ya kupokea wafanyakazi wa mashirika ya kigeni ya kutoa misaada , ikisema kuwa inashughulikia mzozo huo kwa uwezo wake binafsi.
Wakati huo huo kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameliambia shirika la habari la Ujerumani kuwa nchi hiyo itajiunga na Ufaransa katika kumtaka katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon kuitisha mkutano wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuhusu mzozo huo.






