News | 09.05.2008 | 14:00 UTC
Mbeki kuwa na mazungumzo na viongozi wa Zimbabwe.
Harare.
Mpatanishi mkuu katika mzozo wa Zimbabwe rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini , amewasili leo mjini Harare kwa mazungumzo na rais Robert Mugabe kwa ziara yake ya kwanza tangu kutangazwa rasmi matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais.
Mbeki ambaye anakosolewa kwa kuchukua msimamo laini dhidi ya rais Robert Mugabe, anatarajiwa kukutana na kiongozi huyo mkongwe wa Zimbabwe, lakini haijafahamika iwapo atakutana pia na upande wa upinzani.Kiongozi wa chama cha MDC Morgan Tsvangirai hivi sasa yuko nje ya nchi hiyo akikutana na viongozi wa Afrika pamoja na wanadiplomasia katika juhudi za kuongeza mbinyo dhidi ya Mugabe mwenye umri wa miaka 84 kujiuzulu baada ya miaka 28 ya utawala wake.
Chama cha MDC pia kimesema kuwa hakipangi kushiriki katika uchaguzi wa duru ya pili. Tsvangirai hajatoa jibu kamili iwapo atashiriki katika uchaguzi huo na iwapo hatatoa jibu kamili Mugabe mwenye umri wa miaka 84 atakuwa mshindi moja kwa moja.
Pia chama cha MDC kimesema kuwa hadi sasa hakijapata mwaliko kutoka kwa Mbeki kukutana na uongozi wake katika ziara yake ya siku moja mjini Harare.






