1. main content
  2. main navigation
  3. extra content
  4. head navigation
  5. search
  6. Choose form 30 Languages



 

News | 16.05.2008 | 15:00 UTC

Bush - Israel yaweza kuitegemea Marekani.

Jerusalem.


Rais  Bush  wa  Marekani  ameliambia  bunge  la Israel  kuwa  Marekani  itasimama  pamoja  na  Israel katika  kuipinga  Iran  iwapo itajaribu  kujipatia  silaha za  kinuklia.

Bush  ameongeza  kuwa  anakichukulia  kwa umuhimu  wa  juu  kitisho kilichotolewa  na   rais  wa Iran  Mahmoud  Ahmedinejad  kuifuta  Israel  kutoka katika  ramani  ya  dunia. Akizungumza  umuhimu wa  kuitetea  Israel  katika  mashariki  ya  kati  Bush amesema.


O-Ton  Bush


Iran  imesema   kuwa  mpango  wake  wa  kinuklia una  lenga  katika  matumizi  ya  umeme.

Bush,  ambaye  yuko  katika  ziara  kuadhimisha kuasisiwa  kwa  taifa  la  Israel  miaka  60  iliyopita, ameliambia  bunge  la  Israel , Knesset  kuwa  Israel pia  inaweza  kutegemea uhusiano  usiolegalega  na Marekani.

Rais  Bush  ameondoka  nchini  Israel  alielekea nchini  Saudi  Arabia  leo  kuanza  ziara   nchini humo , ambayo  itakuwa  ni  maadhimisho  ya  miaka 75 ya  uhusiano  baina  ya  Marekani  na  nchi  hiyo ya Kifalme.

Bin Laden awashutumu viongozi wa mataifa ya magharibi kuhusu miaka 60 ya Israel

Dubai.


Kiongozi  wa   kundi  la  kigaidi  la  Al-Qaeda  Osama bin Laden  amewashambulia   viongozi  wa  mataifa ya  magharibi  kwa  kushiriki  katika  maadhimisho  ya miaka  60  ya  kuasisiwa  kwa  taifa  hilo  la  Kiyahudi.

Akizungumza  katika  ujumbe   wa  katika  radio  leo Ijumaa , bin Laden  ameapa  kuendeleza mapambano  dhidi  ya  taifa  hilo  la  Kiyahudi pamoja  na  washirika  wake  na  kwamba  Waislamu hawatasalim amri  hadi  pale  Palestina itakapokombolewa  kabisa.

Ujumbe  huo  leo  umekuja  wakati  rais  wa Marekani  George  W. Bush  anakamilisha  ziara yake  nchini  Israel  kuadhimisha  miaka  60  tangu kuasisiwa  kwa  taifa  hilo.

Bin Laden  amesema  katika  ujumbe  huo  kuwa mapambano  kwa  ajili  ya  Palestina  ni  jambo linalosukuma  vita  vya Al-Qaeda  dhidi  ya  mataifa ya  magharibi.

Rais wa China aenda katika eneo la tetemeko.


Beijing.


Rais  wa  China  Hu Jintao amekwenda  katika  mji wa  Mianyang  katika  jimbo  la  Sichuan  kuona binafsi  maafa   yaliyotokea  siku  ya  Jumamosi baada  ya  tetemeko  la  ardhi  kutokea  katika  eneo hilo.

Vyombo  vya  habari  vya  serikali   vimeripoti  kuwa rais  Hu  ametoa  wito  wa  kuongezwa  juhudi  katika kile  alichokieleza  kuwa  ni  awamu  muhimu  ya operesheni  ya  uokozi.

Maafisa  sasa  wanasema ,   wanahofu   kuwa  idadi ya  watu  waliokufa  inaweza  kuwa  juu  zaidi  ya 50,000.

Hadi  sasa , kiasi  cha  watu  22,000  wamethibitishwa kuwa  wamefariki, lakini  watu  wengine  kwa  maelfu hawajulikani  waliko. Mji  wa  Mianyang  umekuwa kituo  cha  kupokea  watu  walionusurika wanaomiminika  kutoka  katika   maeneo yaliyoathirika  karibu  na  eneo  tetemeko  hilo lilipotokea  kilometa  100  upande  wa  magharibi.

Kamishna wa umoja wa Ulaya wa misaada aenda Burma.


Rangoon.


Kamishna  wa  maendeleo   wa   umoja  wa  Ulaya ameutaka  utawala  wa  kijeshi  wa  Burma kuruhusu  wafanyakazi  wa  kutoa  misaada  kuingia nchini  humo  ili  kusaidia   wahanga  wa  kimbunga kilicholeta  maafa  makubwa.

Afisa  wa  umoja  wa  Ulaya   amesema   kuwa   Louis Michel  ametumia  mkutano  wake  na  maafisa  wa kijeshi  wa  utawala  wa  Burma  mjini  Rangoon kuutaka  utawala  huo  kutoa  visa kwa  wataalamu wa   kutoa  misaada  wa  umoja  wa  Ulaya   pamoja na  uhuru  wa  kusafiri  kwa  mashirika  ya  kutoa misaada  ya  umoja  wa  Ulaya.

Michel  ameomba  kufanya  mkutano  na   waziri mkuu  wa  Burma  pamoja  na  waziri  wa  mambo  ya kigeni, na  kuomba  ruhusa  ya  kutembelea  eneo lililoshambuliwa  na  kimbunga  hicho  la Irrawaddy, ambalo  liliathirika  sana   na   kimbunga  Nargis karibu  wiki  mbili  zilizopita.

Mashirika  ya  kimataifa  ya  kutoa  misaada yamesema   kuwa  wahanga  milioni  2.5   wa kimbunga  hicho  wanahitaji  msaada   wa  haraka. Idadi  rasmi  ya  watu  waliokufa  hadi  sasa  imefikia 43,000, lakini  mashirika   ya  kimataifa  yanasema kuwa  idadi  halisi  inaweza  kuwa  zaidi  ya  watu 100,000.

Mzozo wa Chavez na Merkel wagubika mkutano wa L.America.


Lima.


Kansela  wa  Ujerumani  Angela  Merkel  ameahidi msaada  kutoka  Ujerumani  kwa  ajili  ya  wizara  ya mazingira  nchini  Peru  wakati  wa  mkutano  na  rais wa  nchi  hiyo, Alan Garcia.

Kufuatia  mazungumzo  ya  viongozi  hao  wawili, Garcia  ameeleza  kumuunga  kwake  mkono  Merkel katika  mvutano  wake  wa  hivi  karibuni  na  rais  wa Venezuela  Hugo  Chavez.

Merkel  anatarajiwa  kukutana   na  Chavez , kandoni mwa  mkutano   wa  umoja  wa  Ulaya   na  mataifa ya  Latin  Amerika  unaofanyika  leo  Ijumaa  katika mji  mkuu  wa  Peru  , Lima.

Mkutano  huo  unatarajiwa  kujadili  umasikini  na mabadiliko  ya  hali  ya  hewa, lakini  umegubikwa  na mzozo  kati  ya  viongozi  hao  wa  Ujerumani  na Venezuela. Merkel  amezitaka  nchi  za  eneo  hilo kujiweka  mbali  na  serikali  ya  kisishalist  ya Venezuela, wakati  Chavez  amemshutumu  Merkel kwa   kuwa  katika  utamaduni  ule ule  wa  kisiasa wa   enzi  za  Nazi.

uchaguzi wa duru ya pili Zimbabwe Juni 27

Harare.


Tume  ya  uchaguzi  nchini   Zimbabwe   imesema leo  kuwa  uchaguzi  wa  rais  wa  duru  ya  pili utafanyika  Juni  27.

Kiongozi  wa  upinzani  Morgan  Tsvangirai anatarajiwa   kurejea  nchini  Zimbabwe kesho Jumamosi baada  ya   kuwapo  nje  ya  nchi  hiyo kwa  muda  wa  zaidi  ya  mwezi  mmoja  kufuatia uchaguzi  unaobishaniwa.

Tsvangirai  ambaye  hivi  sasa  yuko  nchini  Ireland ya  kaskazini, anatarajiwa  kurejea  nchini  humo  na atawasili  mjini  Harare  mchana, kwa  mujibu  wa mkurugenzi  wa  habari wa  chama  cha  MDC  Luke Tamborinyoka.

Baada  ya  uchaguzi  wa  March  29  kumekuwa  na ghasia  ambapo  chama  cha  upinzani  cha  MDC , kinalaumu  wanajeshi  wa  utawala   utawala  wa Zimbabwe.

Chama  cha  upinzani  kinasema  wanachama  wake 40  wameuwawa  na  zaidi  ya  nyumba   1,000 zimeharibiwa  ama  kuvunjwa.

Chama  cha  ZANU -PF  cha  rais  Robert  Mugabe kimekanusha  kuhusika  na  kukilaumu  chama  cha MDC kwa  kuanzisha  ghasia  katika  juhudi  za kulichafua  jina  la  rais  Mugabe.

Umoja wa mataifa kurejea Somalia.

New York.


Baraza  la  usalama  la  umoja  wa  mataifa limepitisha  azimio  ambalo  linaweza  kufungua   njia kuwekwa  kwa   wanajeshi  wa  umoja  wa  mataifa wa  kulinda  amani  nchini  Somalia.

Licha  ya  kuwa  maandishi  ya   azimio  hilo  hayatoa ahadi  ya  kuwekwa  kwa  jeshi  la  umoja  wa mataifa, lakini  linatoa  wito  kwa  umoja  wa  mataifa kupanga  kuchukua  jukumu  la  ujumbe  wa kulinda  amani  ambao  kwa  sasa  unaendeshwa  na umoja  wa  Afrika.

Pia  azimio  hilo  linatoa  wito  kwa  taasisi  hiyo  ya dunia  kurejesha  operesheni  zake  za  kisiasa katika  nchi  hiyo  iliyoharibiwa  na  vita kutoka  nchi jirani  ya  Kenya. Serikali  ya  Somalia  inayoungwa mkono  na  Ethiopia, imekuwa  ikipambana   na wapiganaji  wa  Kiislamu  tangu  mwaka  2006.

Mkutano wa mataifa ya Ulaya na latin Amerika waanza.

Lima.


Viongozi  kutoka  mataifa  50  ya  Ulaya , Amerika  ya kusini  na  Caribik, wanakutana   mjini  Lima , Peru kujadiliana  kuhusu umasikini, mabadiliko  ya  hali  ya hewa   na  kuongezeka  kwa  bei  za  vyakula duniani. mkutano  huo  huenda  ukashindwa  kufikia makubaliano  juu  ya  majadiliano  ya  kibiashara.

Tayari  kikao  hicho  cha  leo na  kesho kimefunguliwa  kwa  mabishano  miongoni  mwa viongozi  wa  eneo  hilo  kuhusiana  na  biashara huria.

Halikadhalika  malumbano  kati  ya  rais  Hugo Chavez  na  kansela  wa  Ujerumani  Angela Merkel.Mwenyeji  wa  mkutano  huo  rais  Alan Garcia wa  Peru, amesema  viongozi  pia  watajadiliana  juu ya  hali  za   kibinadamu.

Ameongeza   kuwa  masuala  yatakayozingatiwa  ni pamoja  na  hali  za  binadamu  katika  maendeleo ya  teknolojia, utajiri  na  demokrasia  pamoja  na hali  bora  za  kiutu.Rais  Garcia  pia  amemtetea kansela  wa  Ujerumani  Angela  Merkel  katika malumbano  yake  na  kiongozi  wa  Venezuela Hugo Chavez.


O-Ton  Garcia.


Hata  hivyo kansela  wa  Ujerumani  amesema  kuwa anataka  kuimarisha  ushirikiano  wa  kimkakati  na eneo  hilo  na  pia  kuwa  na  masikilizano  na Chavez  katika  kikao  cha  leo  kitakachofanyika pembezoni  mwa  mkutano  huo.

Mivutano  inayoongezeka  kati  ya  viongozi  wa  eneo hilo  la  Amerika  ya  kusini  inatishia  kugubika makubaliano  yoyote  ya  mwisho.

Viongozi hasimu wa Lebanon kukutana Qatar.

Beirut.


Viongozi  wa  makundi  hasimu  ya  kisiasa  nchini Lebanon  wanatarajiwa  kukutana  nchini  Qatar  kwa mazungumzo  yenye  lengo  la  kutatua  mzozo ambao  umeisukuma  nchi  hiyo  katika  ukingo  wa vita  vipya   vya  wenyewe  kwa  wenyewe.

Mkutano  huo  ni  sehemu  ya  makubaliano yaliyopatanishwa  na  jumuiya  ya  nchi  za  Kiarabu siku  ya  Alhamis, ambayo  yamemaliza  mapigano baina  ya  wapiganaji  kutoka  kundi  la  upinzani  la Washia  la  Hezboullah  na  waungaji  mkono  serikali inayoungwa  mkono  na  mataifa  ya  magharibi.

Zaidi  ya  watu  60  wameuwawa  na  wengine  kadha wamejeruhiwa  katika  mapigano  mabaya  kabisa kuwahi  kutokea  nchini  Lebanon  tangu  wakati  wa vita  vya  mwaka  1975-1990.

Mapigano  hayo  yalizushwa  na  hatua  za  serikali kuzuwia  nguvu  za  kundi  la  Hezboullah.

Serikali  imefuta  hatua  hizo. mzozo  wa  kisiasa ulianza  mwishoni  mwa  mwaka  2006  wakati mawaziri  wanaounga  mkono  Syria  walipotoka katika  baraza  la  mawaziri.

Nchi  hiyo  imekuwa  bila  kiongozi  wa  serikali  tangu pale  muda  wa  rais  wa  zamani  Emile  Lahoud ulipomalizika  Novemba  mwaka  jana. Bunge  la nchi  hiyo  limeshindwa  hadi  sasa  kumchagua mrithi  wake.

dalai Lama atoa wito wa kujitawala zaidi Tibet

Bochum, Ujerumani.


Kiongozi  wa  kidini  wa  Tibet  Dalai  lama anaendelea  na  ziara  yake  ya  siku  tano  nchini Ujerumani  akiwa  katika  mji  wa  Bochum.

Kiongozi  huyo  wa  kidini  amewashukuru  waungaji wake  mkono  katika  bara  la  Ulaya  wakati  kwa mara  nyingine  tena  amesisitiza   kuwa  anatafuta kujitawala  zaidi  kwa  jimbo  lake  la  Tibet, na  sio uhuru  kamili.

Jana  Alhamis  Dalai  Lama  alikutana  na  viongozi wa  kisiasa  wa  eneo  la  Ulaya   pamoja  na   rais wa  bunge  la  Ujerumani, Nobert  Lammert.

China  tayari  imepinga   mipango  ya  kukutana  siku ya  Jumatatu  na  waziri  wa  maendeleo  wa Ujerumani  Heidemarie Wieczorek-Zeul.

Mwaka  jana  kansela  Angela  Merkel  alikutana  na Dalai  Lama  mjini  Berlin,  hatua  ambayo ilisababisha  uhusiano  kati  ya  China  na  Ujerumani kuingia  dosari.