Print

 | 24.07.2008 | 03:00 UTC

Wasudan elfu 60, bado wahofia kurejea katika mji wa Abyei.

Umoja wa Mataifa:

Watu wapatao elfu 60, wanakadiriwa kuwa, bado hawawezi kurejea makwao, zaidi ya miezi miwili sasa, tangu kukimbia ghasia zilizotokea katika mji wenye utajiri wa mafuta wa Abyei kusini mwa Sudan.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch, kanda ya Afrika, Geogette Gagnon, raia wengi wanaaminika kuishi katika makazi ya dharura kwenye kitongoji cha Twic kusini mwa Abyei, wakiogopa kurudi kwao, mpaka pale jeshi la Sudan litakapoondoka.

May 13, jeshi la Sudan lilipambana na jeshi la Sudan ya Kusini na kusababisha uharibifu mkubwa huku raia watu wapatao 89 wakiuawa.

Tarehe saba ya mwezi uliopita, wawakilishi kutoka Sudan ya kusini na Kaskazini walikutana kusuluhisha mzozo huo pamoja na kujaribu kuharakisha kurudi kwa raia hao.

Lakini hata hivyo, mpaka sasa hakuna jeshi kati ya hayo, lililoweza kuondoa askari wake wote.


 

Barack Obama kukutana na kansela wa Ujerumani leo.

  Berlin:

Mgombea Urais wa Marekani, kupitia chama cha Democtratic, seneta Barack Obama, leo anaanza ziara yake barani Ulaya, kwa kutembelea Ujerumani, akitokea Israel, mashariki ya kati.

Akiwa mjini Berlin, Seneta Obama atakutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pamoja na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.

Baada ya mazungumzo na viongozi hao, Barack Obama anatarajiwa kutoa hotuba muhimu, kuhusu uhusiano kati ya Ulaya na Marekani katika mkutano wa hadhara, utakaofanyika katikati ya jiji la Berlin leo jioni.

Baadaya kuitembelea Ujerumani, Barack Obama ataendelea na ziara yake barani Ulaya, kwa kuelekea Ufaransa, na baadaye Uingerezai. 


  

Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, zatakiwa kuishinikiza Myanmar kuimarisha haki za binadamu.

SINGAPORE:

Waziri wa Mambo ya Nchi za nje wa Marekani, Condoleeza Rice ametoa wito kwa nchi za Kusini mashariki mwa bara la Asia, kuushinikiza zaidi utawala wa Myanmar, kuimarisha haki za binadamu na kuleta mabadiliko katika demokrasia.

Akizungumza baada ya mkutano wake na Mawaziri wa Nje wa nchi 10 wanachama wa Jumuia ya nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, Condoleeza Rice amesema nchi hizo zinapaswa kuushinikiza utawala huo kuwaachilia wafungwa wa kisiasa, akiwemo mshindi wa tuzo ya Nobel, Aung San Suu Kyi.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, amesema njia nzuri ya Jumuia hiyo ya nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, kuweza kuwa imara zaidi ni kupanua demokrasia na kufuata utawala wa sheria miongoni mwa wanachama wake.

Nchi zinazounda jumuia hiyo ni Malaysia, Phillippines, Singapore, Thailand, Cambodia, Laos, Brunei, Vietnam, Indonesia na Myanmar.


 

Tetemeko la ardhi lajeruhi watu zaidi ya 100, Japan.

Tokyo:

Zaidi ya watu 109 wamejeruhiwa nchini Japan, baada ya tetemeko la ardhi lenye kipimo cha 6.8 kukumba eneo la pwani, kaskazini mwa nchi hiyo.

Polisi nchini humo wamesema kuwa, watu 15 kati ya hao waliojeruhiwa, wako katika hali mbaya.

Tetemeko hilo limetokea katika ukanda wa pwani wa Iwate, kilomita karibu 450 kaskazini mashariki mwa Tokyo.

Tetemeko hilo pia limesababisha nyumba takriban elfu 10, kubaki bila ya umeme kwa muda na nyingine 500 bila ya maji baada ya mabomba kupasuka.

Hata hivyo idara ya utabiri ya hewa nchini humo, imesema hakuna hatari ya kutokea kwa Tsunami, na kwamba pia hakuna madhara yoyote yaliyotokea katika mitambo wa nyuklia iliyoko katika majimbo ya Miyagi na Fukushima.


Utawala wa Bush watoa kipaumbele kwa Iraq.

 WASHINGTON:

Marekani imesema katika kipindi cha mwaka huu, haiwezi kutuma vikosi vya nyongeza vya jeshi nchini Afghanistan.

Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani, imesema kuimarika kwa hali ya ulinzi nchini Iraq, kumeongeza matumaini ya kupeleka vikosi vya jeshi nchini Aghanistan mwakani, lakini kwa sasa Iraq imebaki kuwa kipaumbele cha kwanza kwa utawala wa Rais Bush.

Kamanda wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan alitoa ombi la kupelekwa vikosi zaidi, karibu wanajeshi elfu 10, ili kuweza kupambana na vikundi vya wapiganaji katika maeneo ya mashariki na kusini mwa nchi hiyo.

Awali mgombea Urais wa Marekani kupitia chama cha Democtratic, Barack Obama alisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo, atatoa kipaumbele kwa Afghanistan.

Kwa upande wake, mgombea mwingine wa Urais nchini humo kupitia chama cha Republican, John McCain alieleza kuwa mafanikio nchini Iraq ni muhimu zaidi, lakini alisema pia atatuma vikosi zaidi nchini Afghanistan.

Rais George W Bush wsa Marekani, alikutana na Waziri wake wa ulinzi Robert Gates na maafisa wengine wa jeshi la nchi hiyo, kuzungumzia Iraq na Afghanistan.

Mpaka sasa kuna wanajeshi wa Marekani wapatao elfu 37 nchini Afghanistan, wakati nchini Iraq ni laki moja na elfu 48.


Print